TFF:Bodi ya Ligi kukusanya maoni Udhamini wa Timu zaidi ya moja

Filed in HABARI by on August 23, 2024 0 Comments

TFF:Bodi ya Ligi kukusanya maoni Udhamini wa Timu zaidi ya moja

Bodi ya Ligi Tanzania Bara imefungua milango kwa wadau wote wa soka kutoa maoni yao kuhusu suala la mdhamini mmoja kudhamini zaidi ya timu moja katika Ligi Kuu Tanzania Bara. Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi hiyo, Almasi Kasongo, amesema kuwa kumekuwa na mijadala na hoja miongoni mwa wadau wa soka wakihitaji kuwepo kwa kanuni mpya inayozuia mdhamini mmoja kuwa na udhamini kwa timu zaidi ya moja.

Kasongo alieleza kwamba, licha ya mijadala hiyo kuibuka, kwa sasa hakuna kanuni rasmi inayozuia mdhamini mmoja kudhamini zaidi ya timu moja. Alisisitiza kwamba Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi wanazingatia uwazi na usikivu katika uendeshaji wa soka, hivyo wako tayari kupokea maoni kutoka kwa wadau juu ya suala hili kwa ajili ya msimu ujao.

“Tumeshuhudia mjadala mkubwa katika siku za hivi karibuni, lakini kwa sasa hakuna kanuni inayokataza mdhamini mmoja kudhamini timu zaidi ya moja. Kanuni ni muhimu, lakini ni muhimu zaidi kwa klabu, timu, wachezaji, waamuzi, na viongozi,” alisema Kasongo.

Pamoja na hayo, Kasongo alieleza kuwa maoni ya wadau yatasaidia katika mchakato wa kuunda kanuni mpya kwa msimu ujao, kwani msimu huu tayari umeanza na hakuna mdau aliyewasilisha malalamiko rasmi kuhusu suala hili.

“Kanuni siyo kitu kisichobadilika. Ikiwa wadau wataona umuhimu wa mabadiliko, milango iko wazi kwa maoni na mapendekezo yao. Sisi kama viongozi wa soka, tunataka kuongoza kwa namna ambayo inakubalika na wadau wetu, na tunathamini michango yao,” aliongeza Kasongo.

Kwa mujibu wa Kasongo, lengo kuu ni kuhakikisha kuwa uendeshaji wa soka unafanyika kwa uwazi na kuzingatia maoni ya wadau ili kuboresha michezo nchini.

About the Author ()

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *